Back to news

SYK Foundation Updates

SYK Foundation Yaunga Mkono Elimu Kibaha Kupitia Ziara ya Uongozi na Msaada wa Maendeleo Shuleni

December 15, 2025 · SYK Admin

SYK Foundation Yaunga Mkono Elimu Kibaha Kupitia Ziara ya Uongozi na Msaada wa Maendeleo Shuleni

Katika kuendelea kutekeleza dhamira yake ya kuinua elimu na kuwekeza katika kizazi cha baadaye, SYK Foundation, kwa kushirikiana na wadau wake wa maendeleo, imefanya ziara maalum katika Shule ya Sekondari Mwanalugali, iliyopo Kibaha Manispaa, Mkoa wa Pwani.

Ziara hiyo iliongozwa na Bw. Oscar Mgaya, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya TMRC, ambaye alitembelea shule hiyo kwa niaba ya ushirikiano wa maendeleo unaolenga kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi. Katika ziara hiyo, Bw. Mgaya aliambatana na Dr. Charles Mwamwaja, ambapo walipata fursa ya kuzungumza na walimu pamoja na wanafunzi, wakisisitiza umuhimu wa elimu, nidhamu, na kujituma kama msingi wa mafanikio ya maisha.

picha-ya-pamoja-syk-tmrc-kibaha-secondary.jpeg

Akizungumza mbele ya wanafunzi, Bw. Mgaya aliwahimiza kujiamini, kuthubutu kuota ndoto kubwa, na kutumia elimu kama nyenzo ya kubadili maisha yao na jamii kwa ujumla. Aidha, viongozi wa shule walipata nafasi ya kubadilishana mawazo kuhusu changamoto na fursa zilizopo katika kuboresha maendeleo ya shule.

Kama ishara ya dhamira ya dhati katika kusaidia maendeleo ya elimu, TMRC kupitia ushirikiano na SYK Foundation, ilitoa mchango wa Shilingi milioni 10 (Tsh 10,000,000) kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Shule ya Sekondari Mwanalugali. Msaada huo unalenga kuongeza nguvu katika kuboresha miundombinu na kuweka mazingira bora zaidi ya kufundishia na kujifunzia.

Uongozi wa shule ulitoa shukrani za dhati kwa SYK Foundation na TMRC kwa kuendelea kuwa wadau wa kweli wa elimu, wakisisitiza kuwa mchango huo utakuwa na mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha taaluma na motisha kwa wanafunzi.

Kupitia juhudi kama hizi, SYK Foundation inaendelea kuthibitisha imani yake kwamba elimu ni msingi wa maendeleo endelevu, na kwamba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inawezekana kuleta mabadiliko chanya na ya kudumu katika jamii.